Public Awareness

Historia ya Bima ya Amana

Bima ya Amana ni moja kati ya njia zinazotumiwa na serikali kukuza utulivu wa mfumo wa benki na hivyo kuchangia utulivu wa mfumo wa kifedha. Ni sehemu ya nyongeza katika mtandao mpana wa mfumo wa usalama wa kifedha unaohusisha sheria na kanuni za kibenki, benki kuu kama mkopeshaji wa mwisho na usimamizi wa benki. Mifumo ya Bima ya Amana inakusudiwa kuwalinda wenye amana ndogo kutokana na hasara zinazotokana na kuanguka kwa taasisi za kibenki.

Mfumo wa Bima ya Amana ulianzishwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani mwaka 1933 kufuatia Mdororo Mkubwa wa Uchumi duniani (The Great Depression). Tangu wakati huo, Bima ya Amana imeanzishwa katika nchi zaidi ya 100 katika mabara yote. Katika nchi nyingi, lengo kuu la mfumo wa bima ya amana limekuwa ni kuwakinga wenye amana ndogo katika benki na taasisi za fedha kutokana na hasara inayoweza kutokea benki ikifungwa kwa kuwa hawana uwezo wa kuchanganua ipasavyo taarifa za fedha katika benki na taasisi za fedha wanakoweka amana zao.

Bima ya Amana nchini Tanzania

Mageuzi ya sekta ya fedha ya miaka ya 1990 nchini yalitambua umuhimu wa Mfumo wa Bima ya Amana kwa lengo la kuchangia katika utulivu wa sekta ya fedha na kuongeza imani ya umma katika mfumo wa fedha. Pia, katika kipindi hicho benki binafsi na taasisi za fedha za hapa nchini na za kigeni ziliruhusiwa kuendesha shughuli zake kwa misingi ya uchumi wa soko.

Bodi ya Bima ya Amana (DIB) na Mfuko wa Bima ya Amana vilianzishwa chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991.  DIB ilianza kazi zake rasmi mwaka 1994 chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania. Majukumu ya msingi ya DIB ni kuandaa sera, usimamizi na udhibiti wa Mfuko wa Bima ya Amana na Ulipaji wa Fidia kwa wenye amana. Kufuatia kufutwa kwa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 1991, Bodi ya Bima ya Amana inaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa Vifungu 36 hadi 42 vya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Kama ilivyo kwa taasisi nyingine za bima ya amana duniani, jukumu la msingi la DIB ni kuwakinga wenye amana ndogo dhidi ya vihatarishi vya kupoteza amana zao kutokana na benki na taasisi za fedha kuanguka kwa lengo la kudumisha imani ya umma katika mfumo wa kibenki na fedha.