Majukumu makuu

Ili kuwa na mfumo wa Bima ya Amana wenye tija, utekelezaji wa majukumu makuu kama yalivyoainishwa kwenye dhima na dira ndiyo msingi wa uwepo wa DIB. Bodi ya Bima ya Amana inatekeleza majukumu makuu mawili kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya 2006 ni kusimamia mfuko wa Bima ya Amana na ulipaji wa fidia kwa wenye amana katika benki na taasisi za fedha.

Usimamizi wa Mfuko wa Bima ya Amana

  • Bodi ya Bima ya Amana inakusanya michango ya kila mwaka kutoka benki na taasisi za fedha. Kwa hivi sasa, benki na taasisi za fedha huchangia kiasi kinacholingana na 1/10 ya asilimia 1.5 ya wastani wa amana zote kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
  • Bodi ya Bima ya Amana inawalipa wenye amana katika benki iliyofutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania, na
  • Bodi inaweza kusimamia ufilisi wa benki au taasisi ya fedha iliyofutiwa leseni kama ikiteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Mfuko wa Bima ya Amana ulipokea mchango wa shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na Serikali wakati wa kuanzishwa Mfuko mwaka 1994. Mfuko unaendelea kukua kutokana na michango ya kila mwaka kutoka kwa wanachama (mabenki na taasisi za fedha), na faida inayotokana na uwekezaji katika dhamana za serikali.

Ulipaji wa Fidia kwa wenye Amana

Jukumu la Bodi ya Bima ya Amana ni kuwalinda wenye amana dhidi ya athari ya kupoteza amana zao pale benki au taasisi ya fedha inapowekwa katika ufilisi (kwa mujibu wa sheria). Kufanya hivyo kunaifanya jamii kuendelea kuwa na imani na mfumo wa fedha nchini. Kwa hivi sasa, kiwango cha juu cha kinga ni shilingi za Tanzania milioni 1.5 kwa kila mwenye amana katika kila benki au taasisi ya fedha. Kiwango hiki kinakidhi asilimia 95 ya amana zilizokingwa.

Fund Management Vorious Photo