Public Awareness

Ufilisi

Utangulizi

Inapoteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kuwa mfilisi, DIB inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 41 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Kwa sasa, DIB inafilisi jumla ya benki tisa (9) ambazo zilifungwa na BOT katika nyakati tofauti. Benki zilizoanguka na ambazo ziko chini ya ufilisi ni: Greenland Bank Tanzania Limited (2000); Delphis Bank Tanzania Limited (2003); FBME Bank Limited (2017); Mbinga Community Bank Plc (2017); Njombe Community Bank Limited (2018); Meru Community Bank Limited (2018); Covenant Bank for Women (T) Limited (2018); Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited (2018) na Efatha Bank Limited (2018).

Zoezi la ufilisi wa Greenland Bank (T) Limited na Delphis Bank (T) Ltd lipo katika hatua za mwisho; wakati zoezi la ufilisi wa benki nyingine saba zilizofungwa linaendelea.

Mara baada ya kuteuliwa kama mfilisi, DIB huanza kwa kulipa fidia ya amana zilizokingwa mara  moja wakati zoezi la ufilisi likiendelea. Kama mfilisi, DIB inakusanya mali na kuwalipa wadai kutokana na kiasi kinachokusanywa kwa mujibu wa vifungu vya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya 2006 na Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002.

Ukusanyaji wa Madeni

Ukusanyaji wa madeni ni moja ya majukumu ya DIB katika zoezi la ufilisi. Kazi hii ni pamoja na kuhifadhi mali zote za benki zilizo katika ufilisi. Ili kutekeleza vizuri zoezi la ufilisi, DIB imekuwa ikifuatilia urejeshwaji wa fedha na wakopaji na wakati mwingine imeajiri wakusanya madeni na kufungua kesi za madai kwa wanaogoma kufanya marejesho ya mikopo waliyochukua. Hata hivyo, zoezi la ukuzanyaji madeni limekumbwa na changamoto kadhaa, zikiwemo kesi na mapingamizi mbalimbali mahakamani dhidi ya mfilisi pamoja na masuala ambayo hayajatatuliwa katika nchi na nchi kuhusu iliyokuwa FBME Bank Limited.

Uuzaji wa Mali

Uuzaji wa Mali unahusisha kuuza mali kwa njia ya minada ya hadhara baada ya kufanya zoezi la tathmini na mali husika kupewa bei za ufilisi. DIB kupitia madalali imefanya minada kadha kwa kila benki ambayo iko katika ufilisi.

Ukusanyaji wa Mali kutoka Vyanzo Vingine

Pia, DIB inakusanya mali kutoka vyanzo vingine ikiwa ni pamoja na kujua salio la amana na uwekezaji katika benki za hapa nchini na za kigeni inazoshirikiana nazo na albaki ya fedha kutokana na miamala ya kadi za kielektroniki (kwa mfano, VISA na MasterCard). Aidha, DIB inawekeza fedha za ziada zilizopatikana kutokana na ukusanyaji wa madeni, uuzaji wa mali na kutoka vyanzo vingine kwenye Dhamana za Serikali na Hati fungani  kwa lengo la kuhifadhi thamani kwa njia ya mapato ya uwekezaji katika riba ya mapato. Mapato husaidia kugharamia ufilisi na kuongeza fedha za ufilisi kwa ajili ya wadai.

Mgawanyo wa Makusanyo ya Ufilisi kwa Wadai

DIB inaendelea kufanya malipo kwa wenye amana wanaoidai kutokana na makusanyo ya zoezi la ufilisi wa benki nne. Uwiano wa mgawanyo wa fedha ziizopo kwa wadai wa benki nne ni kwamba Njombe Community Bank Limited watapata asilimia 100, Meru Community Bank Limited (asilimia 69), Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited (asilimia 43 na Mbinga Community Bank Limited (asilimia 33). Aidha, mchakato wa kuwalipa wenye amana na wadai katika benki nyingine zilizo chini ya ufilisi unaendelea.